Shughuli zaendelea katika afisi za serikali licha ya mwito wa Raila

Kinyume cha mito ya kinara mwenza wa muungano wa upinzani NASA Raila Odinga kwa wafanyikazi kutofika kazini jana, wafanyikazi wote wa serikali katika eneo la Rift Valley walienda kazini kama kawaida. Raila alikuwa ametoa wito kwa wafanyikazi kutoenda kazini jana ili kuomboleza vifo vya waathiriwa wanaodaiwa kupigwa risasi na polisi wakati wa maandamano ya kupinga kutangazwa kwa Rais Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa Urais kwenye uchaguzi wa hivi punde. Kulingana na mshirikishi wa shughuli za serikali katika eneo la Rift Valley Wanyama Musyambo, shughuli za kawaida ziliendelea katika afisi za serikali za kaunty zote 14 za eneo hilo. Musyambo alisema hayo alipozuru sehemu mbali mbali za kaunti ndogo ya Naivasha kufuatia ripoti kwenye mtandao wa kijami kwamba watu fulani waliteketezwa kwenye gari moja la kibinafsi. Musyambo ambaye aliandamana na maafisa wakuu wa usalama alitaja ripoti hizo kuwa za uongo ambazo zinaenezwa na watu wenye nia mbaya. Alisema serikali inawasaka watu waliosambaza ujumbe huo.