Wadhifa Wa Mwenyekiti IEBC Watangazwa Tena

Wadhifa wa mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka umetangazwa tena. Jopo la uteuzi lililopewa jukumu la kuwateua maafisa wapya wa tume hiyo limetoa wito kwa watu walio na ujuzi unaohitajika kuwasilisha maombi kwa wadhifa huo kwenye tangazo lililochapishwa katika magazeti ya humu nchini. Hapo jana mwenyekiti wa jopo hilo Bernadette Musundi alisema kuwa waliafikia uamuzi huo baada ya maswali kadhaa kuibuka kuhusiana an ufaafu wa wale walioorodheshwa baada ya kuwachunguza. Mahojiano kwa wale walioorodheshwa kwa nyadhifa sita za makamishna wa tume hiyo yataendelea jinsi iliyopangwa. Mwaniaji atakayefaulu atateuliwa kwa kipindi kimoja cha miaka sita. Majina ya wale wote waliowasilisha maombi yatachapishwa kwenye vyombo vya habari, gazeti rasmi la serikali, na kwenye tovuti ya tume ya kuwaajiri maafisa wa bunge baada ya kukamilika kwa tangazo hilo. Wakati huo huo mahojiano kwa nyadhifa nyingine yataanza tarehe mosi mwezi ujao. Juhudi za kuwatafuta makamishna wapya wa tume hiyo huenda zikaendelea hadi katikati ya mwezi Januari kwani ni sharti bunge liidhinishe wale watakaoteuliwa na jopo hilo.