Wabunge watatu wa ODM huko Wajir wajiunga na Jubilee

Wabunge watatu wa chama cha ODM huko Wajir leo waliongoza jamii ya Degodia kujiunga na chama cha Jubilee wakisema hawawezi kuendelea kuwa katika upinzani. Wabunge hao watatu ni Adan Keynan Wehliye, Mohammed Ibrahim Elmi na Abass Sheikh Mohammed. Viongozi hao ambao walijumuisha waakilishi 15 wa wodi katika kaunti hiyo wakiongozwa na spika wao Bishar Omar walisema uamuzi wao wa kujiunga na chama tawala umetokana na ajenda ya maendeleo inayotekelezwa na serikali kote nchini. Mbunge wa Eldas, Adan Keynan, alisema kaunti ya Wajir iliamua kujiunga na chama tawala kwani huo ndio upande utakaoshinda kwenye uchaguzi mkuu ujao. Viongozi hao ambao walikuwa wakiongea katika Ikulu ya Nairobi, walisema kaunti hiyo imeathiriwa pakubwa na hali ya ukame inayojiri kwa sasa na wakahimiza serikali kuimarisha mpango wake wa kukabiliana na ukame katika kaunti hiyo. Akiongea wakati wa hafla hiyo, rais Uhuru Kenyatta alisema imekuwa azma yake kushirikiana na watu wa Wajir kwa minajili ya kuimarisha umoja na uthabiti katika eneo hilo. Rais alisema serikali inatekeleza miradi kadhaa ya maendeleo huko Wajir inayodhamiriwa kuimarisha viwango vya maisha vya wakazi wa kaunti hiyo.