Wabunge Watatu Wa CORD Wahojiwa Kuhusiana Na Matamshi Ya Chuki

Wabunge watatu wa mrengo wa CORD wanahojiwa kwenye makao makuu ya idara ya upelelezi wa jinai kuhusiana na matamshi ya chuki na uchochezi. Viongozi wa muungano huo Raila Odinga na Kalonzo Musyoka pia wamefika mahali hapo kuungana na wabunge hao. Wabunge hao walijisalimisha kwenye idara hiyo baada ya sarakasi kutokea leo asubuhi wakati mbunge wa Suna mashariki Junet Mohamed alipochukuliwa unyo unyo pamoja na mawakili wake na maafisa wa kikosi cha Flying Squad kutoka jumba la Nation Centre jijini ambapo alikuwa akishiriki kipindi cha mazungumzo ya moja kwa moja. Seneta wa kaunti ya Machakos Johnstone Muthama alijisalimisha baada ya maafisa wa kikosi hicho kukita kambi nje ya nyumba yake katika mtaa wa Runda usiku kucha. Kwa upande wake, mbunge wa Kitutu Masaba, Timothy Bosire alisema maafisa wa kikosi hicho waliwasili nyumbani kwake katika mtaa wa Karen ambapo walimtaka kuandamana nao hadi kwenye makao makuu ya idara ya upelelezi wa jinai. Awali, wabunge hao walikuwa wamehoji kuwa hawajapokea mwaliko rasmi wa kufika kwenye idara hiyo kuhojiwa. Polisi pia wanachunguza madai ya matamshi ya chuki dhidi ya wabunge Moses Kuria, Ferdinand Waititu, Kimani Ngunjiri na mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Kilifi, Aisha Jumwa. Waititu na Kuria walifika kwenye idara hiyo hapo jana ambapo walihojiwa na kuachiliwa.