Wabunge wataka mabwanyenye pia waondolewe Mau

Mjadala wa kuwahamisha watu kutoka msitu wa Mau unaendelea kuzua hisia tofauti huku wabunge sasa wakisema wanaomiliki vipande vikubwa vya ardhi na viwanda vya majani chai kwenye msitu wa Mau pia wahamishwe. Kiongozi wa wengi Aden Duale alisema inasikitisha kwamba shughuli inayoendelea ya kuwahamisha watu inawalenga tu wasiojimudu ikilinganishwa na wale walio na ushawishi na wanaendesha shughuli za kibiashara katika msitu wa Mau.

Wabunge ambao walikuwa wakijadili hoja kuhusu usimamizi wa misitu na ukataji miti hapa nchini walisisitiza kwamba shughuli hiyo yapasa kusimamishwa hadi watu matajiri pia watakapoondolewa kutoka msitu huo wenye chemichemi kubwa zaidi ya maji hapa nchini. Hata hivyo wabunge walikubaliana kwamba nchi hii sharti ijizatiti kuhifadhi sehemu zake zenye chemichemni za maji.

Serikali inadhamiria kuwahamisha watu elfu-400 kutoka msitu wa Mau.