Wabunge wanne Jubilee kusalia kwenye kamati wakisubiri kesi inayowakabili

Mahakama kuu imewarejesha kwa muda wabunge wanne wa chama cha Jubilee waliokuwa wameondolewa kwenye kamati kusubiri kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi inayowakabili. Alfred Keter wa Nandi Hills amesema kuwa wataliomba bunge kumwondoa kiongozi wa wengi bungeni Aden Duale na kiranja mkuu Benjamin Washiali. Keter, mbunge wa Moiben Silas Tiren, mwenzao wa Embakasi kaskazini James Gakuya na Kangogo Bowen wa Marakwet mashariki wametaja hatua hiyo kuwa adhabu na awanataka uamuzi huo utupiliwe mbali kwa sababu ya kukiuka haki ya kufikiria miongoni mwa sababu nyingine. Wabunge hao waliondolewa kwenye kamati ya leba na maslahi ya jamii, ile ya mazingira na rasilmali za kitaifa, ile ya kilimo na ufugaji na ile ya kitengo cha bunge cha utangazaji kwa kupinga uteuzi wa chama chao wa mwenyekiti na naibu wake.