Wabunge Wamuenzi Aliyekua Mbunge Wa Malava, Marehemu Soita Shitanda

Kulikuwa na kimya cha dakika moja kwenye bunge la taifa kumuenzi aliyekuwa mbunge wa Malava, Soita Shitanda aliyeaga dunia jumanne iliyopita baada ya kuugua kwa muda mrefu. Spika wa bunge, Justin Muturi alimtaja marehemu Shitanda kuwa mzalendo atakayekumbukwa na wengi. Wabunge waliotuma risala zao za rambi rambi walimtaja Shitanda kuwa mtu aliyeweka mbele maslahi ya wakazi wa Malava. Mbunge wa Matungu, David Were alilieleza bunge kuwa marehemu Shitanda alipigania maslahi ya wakuza miwa katika eneo la magharibi ya Kenya. Mbunge maalum, Amina Abdalla alimkumbuka Shitanda kuwa mtu mcheshi zaidi katika bunge la 10. Na kwenye risala yake, mbunge wa Mumias Mashariki, Benjamin Washiali aliwahimiza wanasiasa kuifariji familia ya mwendazake wakati wa mazishi badala ya kugeuza mazishi kuwa jukwaa la siasa.