Wabunge wahimizwa kudumisha ubora wa mijadala bungeni

Wabunge wamehimizwa kudumisha ubora wa mijadala bungeni na kuhakikisha sheria wanazopitisha zina manufaa kwa Wakenya. Kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa, John Mbadi pia alihimiza mashirika yasiyo ya serikali yanayotathmini utendakazi wa bunge kuzingatia mchango wa mbunge kwenye mijadala hiyo pamoja na ubora na umuhimu wa mchango wake. Mbadi alitoa mfano wa gavana wa sasa wa Vihiga, Wilbur Ottichilo ambaye akiwa mbunge wa Emuhaya aliwasilisha hoja na kuchangia mahusis mijadala inayohusu maswala ya teknolojia na sayansi ya anga wa juu. Mbadi alisema hayo wakati wa mjadala kuhusu hoja ya kutoa mwongozo wa kujadili hotuba ya rais. Maoni yake yaliungwa mkono na naibu spika wa bunge la taifa, Moses Cheboi aliyewahimiza wabunge kutumia tajriba yao katika sekta mbalimbali kuboresha mijadala bungeni. Wabunge pia waliidhinisha kalenda ya mijadala kwenye kikao cha pili cha bunge kilichoanza jana na ambacho kitamalizika tarehe 6 mwezi Disemba mwaka huu.