Wabunge Waghadhabishwa Na Kucheleweshwa Kwa Fedha Za CDF

Wabunge wameeleza kughadhabishwa kwao na kucheleweshwa kwa usambazaji wa pesa zlizotengewa ustawi wa maeneo-bunge. Wakiongozwa na wabunge David Ochieng wa Ugunja, Mary Emase wa Teso Kusini, John Serut wa Mlima Elgon, Nelson Gaichuhie wa Subukia na Robert Pkose wa Endebes, wabunge hao walimtaka mwenyekiti wa hazina ya kitaifa ya ustawi wa maeneo bunge, Moses Lessonet kuelezea sababu za kucheleweshwa kwa pesa hizo katika kipindi cha matumizi ya pesa za serikali cha 2015-2016. Walidai kuwa hatua hiyo imelemaza miradi ya maendeleo.

Wabunge hao walimtaka Lessonet kutoa jawabu kabla ya kuanza kwa mjadala kuhusu pesa zilizotengewa ustawi wa maeneo bunge katika kipindi cha kifedha cha 2016-2017. Baadhi yao walidai kuwa hawajapata hata nusu ya pesa ziliotengewa ustawi wa maeneobunge yao katika kipindi kilichopita cha matumizi ya pesa za serikali. Hata hivyo Lessonet aliwahakikishia wabunge kuwa tayari pesa hizo zimetolewa kwa hazina ya kitaifa ya ustawi wa maeneo bunge kabla ya kuwasilishwa katika akaunti za maeneobunge hayo. Alisema kamati yake tayari imejadiliana na waziri wa fedha Henry Rotich kuharakisha uwasilishaji wa pesa hizo.