Wabunge Wa Zamani Kupokea Shilingi 100,000 Kila Mwezi

Kamati kuhusu fedha, mipango na biashara jana alasiri iliwasilisha taarifa ambayo ikiridhiwa wabunge waliohudumu kati ya mwaka wa 1984 na 2002 watalipwa malipo ya kustaafu ya kila mwezi ya shilingi 100,000. Hiyo inafuatia kuwasilishwa bungeni hapo mwezi Oktoba mwaka uliopita kwa taarifa na mbunge wa Rarieda Nicholas Gumbo kwa niaba ya chama cha wabunge wa zamani nchini (FOPAK) na wabunge wa zamani kuhusu utekelezaji wa taarifa ya jopo la Akiwumi ya mwaka 2009 kuhusu malipo ya chini ya kustaafu kwa wabunge. Wakiunga mkono taarifa hiyo wabunge walisema ni muhimu kuridhia taarifa hiyo ya Akiwumi kabla ya uchaguzi mkuu hapo Agosti 8 wakidai kwamba kati ya asilimia 75 hadi 80 ya wabunge hawatarudi bungeni. Kulingana na wawasilishaji wa taarifa hiyo utaratibu wa kuhudumu wa wabunge haujali maisha yao baada ya kustaafu bungeni, na hivyo wengi wao huathirika kiuchumi. Taarifa hiyo iliridhiwa na bunge hapo Juni 30 mwaka wa 2009 na kuipa jukumu kamati muhimu ya bunge kutekeleza marekebisho muhimu kwa sheria hiyo ili kutekeleza mapendekezo hayo ya taarifa ya jopo la Akiwumi kuhusu malipo ya kustaafu ya wabunge. Walisema kwamba wabunge wa zamani wanaendelea kupata kati ya shilingi 2,700 na 40,000, ambazo haziwakimu kiuchumi . Taarifa ya kamati hiyo itaorodheshwa kwenye taarifa ya kujadiliwa.