Wabunge kujadili pendekezo la rais kuhusu ushuru kwa bidhaa za mafuta

Bunge la kitaifa juma hili litafanya vikao maalum vya siku mbili kujadili pendekezo la Rais Uhuru Kenyatta la kupunguza kwa asilimia 50 ushuru ziada wa thamani VAT kwa bidhaa za mafuta badala ya  kusimamisha utekelezaji wa ushuru huo kwa muda

Vikao hivyo vitaandaliwa siku ya Jumanne na Alhamisi. Katika hotuba yake kwa taifa wiki iliyopita, Rais Kenyatta alisema ameurudisha bungeni mswada huo unaopendekeza kusimamisha kutekelezwa kwa ushuru ziada wa thamani wa asilimia 16 kwa bidhaa za mafuta ya petrol kwa sababu hauonyeshi changamoto zinazoongezeka humu nchini.

Alisema utakuwa na athari hasi kwa ajenda nne kuu za maendeleo ambazo ni afya ya msingi, chakula cha kutosha, kuongeza utengenezaji bidhaa, na nyumba za gharama nafuu. Pendekezo hilo likiidhinishwa na bunge litawezesha bei ya mafuta ya petrol aina ya super kupungua hadi shilingi 118 kwa lita moja ilhali dizeli itagharimu shilingi Sh107 . Ushuru wa VAT kwa bidhaa za mafuta ulianza kutekelezwa Septemba 1, licha ya mswada huo uliofanyiwa marekebisho kupitishwa  na Bunge kutaka usimamishwe.