Wabunge 3 kutoka South Rift wanadai mapigano katika Kaunti za Nakuru, Narok ni za kisiasa

Wabunge watatu kutoka eneo la South Rift wamedai kwamba mapigano kwenye mpaka kati ya kaunti za Narok na Nakuru yanachochewa kisiasa.Wabunge sasa wanataka seneta wa kaunti ya Narok  Ledama Olekina,mbunge wa Narok Kaskazini Moitalel Kenta na aliyekuwa spika wa bunge la kaunti ya Nairobi Alex Magelo kuchunguzwa kuhusiana na ghasia hizo .

Wabunge hao ,Nelson Koech wa Belgut, Hillary Kosgei wa Kipkelion magharibi na Kipsengeret Koros wa Soin-Sigowet,pia wanamtaka rais Uhuru Kenyatta kumfuta kazi waziri wa mazingira Keriako Tobiko,kwa madai ya kuwa na mapendeleo kuhusu swala hilo .

Mtu mmoja ameuawa na wengine 26 kulazwa hospitalini kufwatia mapigano kwenye mpaka kati ya kaunti hizo mbili, huku mamia ya watu wakihama makazi yao na nyumba kadhaa kuteketezwa.