Waathiriwa Wa Ghasia Za Baada Ya Uchaguzi Wa 2007 Wataka Viongozi Wanaoeneza Chuki Wafungwe Gerezanii

Waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 sasa wanataka viongozi wanaoeneza chuki miongoni mwa wakenya wafungwe gerezani. Wakimbizi hao wa ndani kwa ndani walisema taifa hili litakuwa likionyesha mfano mbaya kwa kuwaruhusu viongozi hao kuendelea kueneza chuki miongoni mwa Wakenya wapenda amani. Chini ya vuguvugu la Peace Ambassadors Network, waathiriwa hao wanasema wameteseka kutosha na hawangependa kuona ghasia kama zile zilizokumba taifa hili mwaka 2008 zikishuhudiwa tena. Mwakilishi wa waathiriwa hao Harun Macharia alitoa wito kwa idara ya mahakama kuwachukulia adhabu kali viongozi wanaoeneza chuki ili wawe mfano kwa wengine. Macharia alisema haya wakati wa mkutano wa waathiriwa wapatao 200 wengi wao wakiwa manusura wa mkasa wa moto wa kanisa la Kiambaa katika eneo la Naivasha wakati wa ghasia hizo.