Vyama vya wahudumu wa vyuo vikuu vyafika mbele ya kamati la senate kuhusu mkata wa nyongeza ya mishahara

Vyama vya wahudumu wa vyuo vikuu vilivyofika mbele ya kamati ya Senate kuhusu elimu viliikosoa wizara ya elimu, tume ya mishahara na marupurupu na manaibu wa chansela wa vyuo kwa kuwa vikwazo kwa mashauriano kuhusu mkataba wa nyongeza ya mishahara wa mwaka 2017-2021. Walidai kwamba taasisi hizo hazijawasilisha pendekezo lolote ili kuanzisha mashauriano yanayoweza kukomesha mgomo huo.

Vyama hivyo pia vilisema kuwa vyuo vikuu vya umma havijakuwa vikiwasilisha pesa wanazokatwa wahudumu hao za mpango wa malipo ya uzeeni, bima ya taifa ya matibabu na pia vyama vya ushirika na mikopo ya benki. Walilalamika kwamba wafanyikazi hao na familia zao wamekosa kupata huduma hospitalini kwa sababu pesa hizo hazikuwasilishwa.

Kadhalika walidai kuwa vyuo hivyo vikuu havijawianisha umri wa kustaafu huku baadhi zikiwastaafisha wafadhiri katika umri wa miaka 65 na vingine miaka 75. Vyama hivyo vililihimiza bunge la Senate kuchunguza madai hayo na kupendekeza kuwa mashauriano yoyote yanafaa kuwahusisha maafisa wa wizara ya fedha, afisi ya rais na wizara ya elimu.