Viwavi wasababisha hasara kwa mimea, kaunti ya Isiolo

Wakulima katika kaunti ya Isiolo wana wasi wasi baada ya mimea yao ya chakula kuvamiwa na viwavi.Wadudu hao ambao hula mimea yoyote ya kijani kibichi, waligunduliwa mwanzo katika maeneo ya Gafarsa na Iresaboru na sasa wamesambaa hadi Isiolo ya kati.Wakulima hao sasa wanasema viwavi hao wamevamia afisi za serikali, mashamba na hata makazi ya watu.
Afisa mkuu wa kilimo katika kaunti hiyo Adan Jaldesa amethibitisha uvamizi huo, akisema kuwa ekari zisizopungua 200 za mashamba katika maeneo ya Kakili, Kambi ya juu na Burat zimeharibiwa akihofia kuwa huenda wadudu hao wakasambaa katika kaunti nzima. Hata hivyo, Adan amesema amepokea lita 100 za kemikali ya kuwaua wadudu hao kutoka shirika la kuwalinda mimea na wanatumia dawa hiyo kukabiliana na wadudu hao.