Visa 15 vipya vya covid-19 vyadhibitishwa nchini huku watu watatu zaidi wakiaga dunia

Watu 15 zaidi wameambukizwa virusi vya covid-19 na kufikisha idadi ya wale wanaougua virusi hivyo humu nchini kuwa 715.

Kati ya visa hivyo 15 vilivyoripotiwa Jumanne, 14 ni vya wakenya huku kisa kimoja kikiwa cha raia wa Rwanda.

Akitangaza hayo wakati wa arifa ya kila siku kuhusu virusi vya covid-19 humu nchini, katibu mwandamizi katika wizara ya Afya Dkt Rashid Aman alisema 10 kati ya visa hivyo ni vya wanaume ilhali visa 5 ni vya wanawake.

Waathiriwa wa visa vya Jumanne ni wa umri wa kati ya mwaka mmoja na miaka 62.

Dktr Aman alisema sampuli 978 zilifanyiwa uchunguzi katika muda wa 24 zilizopita.

Wakati uo huo watu nane zaidi wameruhusiwa kuondoka hospitalini baada ya kupona virusi hivyo hatari na kufikisha idadi ya waliopona covid-19 humu nchini kuwa 259.

Hata hivyo wakenya 3 wameaga dunia kutokana na virusi hivyo na kuongeza idadi ya walioaga dunia kufika 36.

Katibu mwandamizi katika wizara ya afya Dkt Rashid Aman alisema wizara yake itapeleka maafisa wake katika mpaka wa Namanga kutathmini hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya covid-19 katka mipaka ya humu nchini.

Siku ya Jumatatu madereva watatu wa masafa marefu wa raia wa kenya waligunduliwa kuugua virusi vya covid-19 katika mpaka wa Namanga.