Virusi vya Chikungunya vyapatikana Mombasa

Watu 32 wamelazwa katika hospitali mbali mbali za umma katika kaunti ya Mombasa baada ya kuambukizwa virusi vya maradhi ya Chikungunya. Kufikia sasa kuna visa 120 vinavyoshukiwa kuwa vya maradhi hayo, ambapo visa 32 vimethibitishwa kuwa vya watu walioambukizwa virusi vya ugonjwa huo. Gavana wa kaunti ya Mombasa, Hassan Joho, kwenye hatua ya dharura ya kuimarisha utathmini wa ugonjwa huo, amezindua magari matano ya kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya ugonjwa huo, mashini mpya na kemikali za kunyunyiziaA�A�makaazi kwenye kaunti hiyo katika juhudi za kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa huo. Joho alisema maeneobunge ya Changamwe na Mvita ndiyo yameathiriwa pakubwa na chamuko la ugonjwa huo.

Kulingana na shirika la afya duniani, maradhi ya Chikungunya yanasambazwa kupitia kwa mbu hadi kwa binadamu. Wakaazi wamehimizwa kushirikiana na serikali ya kaunti kusimamia uzoaji taka ili kuondoa maeneo ambako mbu wanazaana. Ugonjwa wa Chikungunya husababisha homa na maumivu makali ya viungo vya mwili. Dalili nyingine ni pamoja na maumivu ya misuli, kuumwa na kichwa, uchovu na kuchipuka vipele mwilini.