Viongozi wa upinzani wasema kupambana na ufisadi ndio agenda ya NASA

Viongozi wa upinzani wametaja mapambano dhidi ya ufisadi na utatuzi wa dhuluma za kihistoria kuwa baadhi ya ajenda kuu ya muungano wa NASA. Viongozi hao walisema kwamba wataanzisha mazungumzo ya kitaifa ili wakenya waweze kuongeleshana na kukubaliana kuhusu jinsi ya kukabiliana na maswala yanayowagawanya. Aidha walisema hakuna atakayechaguliwa kupitia muungano wa NASA na wale watakaoteuliwa kuhudumu na serikali ya NASA watakaoruhusiwa kufanya biashara na serikali moja kwa moja ama kupitia mawakala ili kuzuia kuingiliana kwa maslahi na kupunguza ufisadi. Aidha viongozi hao walisema kwamba muungano wa NASA umejitolea kuimarisha ugatuzi kwa kuhamisha majukumu yote na fedha katika kaunti wakidai kuwa serikali ya Jubilee inazuia hayo. Kuhusu mabadiliko ya serikali viongozi hao walisema serikali ya muungano wa NASA Coalition itatekeleza mabadiliko yatakayoleta uponyaji wa madhara ya ukoloni ili kila afisa wa umma kuanzia Rais hadi chini wanaangaziwa kwa jukumu walilopewa na wananchi kuwahudumia na wala sio kuwatawala.