Viongozi wa NASA wapeleka kampeni Pwani

Viongozi wa muungano wa NASA wamepeleka kampeni zao katika kaunti za eneo la Pwani. Viongozi hao watakita kambi katika eneo hilo leo na kesho kutafuta uungwaji mkono wa wapigai kura milioni 1.7 katika kaunti-6 za eneo la Pwani. Mgombeaji urais wa muungano wa NASA, Raila Odinga na mgombea-mwenza Kalonzo Musyoka wataongoza kampeni za muungano huo wa upinzani huko Mariakani kabla ya kuelekea Kaloleni, Rabai na Mazeras katika kaunti ya Kilifi. Hatimaye wataelekea katika eneo la Lamu ambako wataungana na Waislamu kwa Iftar. Kiongozi wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi na kiongozi wa wachache katika bunge la seneti, Moses Wetanga��ula watakita kambi katika eneo la Lamu ambako watapigia debe muungano huo. Hapo kesho, Raila na Musyoka watazuru maeneo ya Voi na Taveta katika kaunti ya Taita Taveta. Mudavadi na Wetanga��ula watakuwa katika sehemu za Wundanyi na Mwatate. Makundi hayo mawili kisha yatajumuika Waislamu huko Mombasa kwa Iftar. Ziara ya viongozi wa upinzani katika eneo la Pwani imejiri wiki moja baada ya rais Kenyatta kuzindua reli mpya ya kisasa huko Mombasa. Siku ya jumamosi, viongozi wa NASA watakuwa katika kaunti ya Makueni.