Viongozi Wa Kidini Waitaka Serikali Kukabiliana Na Kuingizwa Kwa Bunduki Kimagendo Nchini

Viongozi wa kidini kutoka kaunti ya Migori wanaitaka serikali ya taifa kuratibu mbinu za kukabiliana na kuingizwa bunduki kimagendo hapa nchini. Viongozi hao ambao walijumuisha, reverend John Chacha wa kanisa la Maranatha, Samuel Maheri wa dhehebu la Apostolic, kasisi John Owino wa kanisa katoliki, mchungaji Peter Omanga wa makanisa ya Seventh Day AdventistA� na Ibrahim Hussein wa dini ya kiislamu walieleza masikitiko kwamba bunduki zinatumiwa katika karibu visa vyote vya uhalifu hali inayobainisha kwamba zinapatikana kwa urahisi. Kwenye taarifa ya pamoja mjini Isebania hapo jana, vongozi hao walitaja mji huo wa mpakani kuwa ulioathiriwa pakubwa na visa vilivyokithiri vya wizi wa kimabavu katika kaunti hiyo. Waliiomba serikali kuratibu mbinu za kuwapokonya silaha wahalifu katika sehemu hiyo. Viongozi hao walisema majambazi wenye bunduki wana ujasiri mwingi na hata hutekeleza wizi wakati wa mchana. Viongozi hao wa kidini walimhimiza waziri wa usalama wa taifa Joseph Nkaissery kuwapa maafisa wa usalama vifaa zaidi vya kuwawezesha kukabiliana vilivyo na wahalifu.