Vifijo na ghasia zaripotiwa baada ya maamuzi ya mahakama

Zilikuwa sherehe katika sehemu mbali mbali za nchi kufuatia uamuzi wa mahakama ya juu wa kudumisha ushindi wa rais Uhuru Kenyatta kwenye marudio ya uchaguzi wa Urais ya tarehe 26 mwezi oktoba. Jijini Nairobi baadhi ya wakenya walishangilia uamuzi huo nje ya mahakama ya juu huku wengine wakisherehekea kwenye barabara za jiji. Sherehe hizo pia zilishuhudiwa katika miji ya Nyeri, Nanyuki, Eldoret na Gatundu ambako wakazi waliandamana kusherehekea ushindi wa Rais hadi nyumbani kwake A�Ichaweri.

Hata hivyo, ghasia zilizuka katika kaunti za Kisumu na Migori na pia katika mtaa wa Mathare jijini Nairobi muda mfupi baada ya mahakama ya juu kudumisha kuchaguliwa tena kwa Uhuru Kenyatta kwenye marudio ya uchaguzi wa urais tarehe 26 mwezi uliopita. Mamia ya wakazi waliandamana kwenye barabara za Kisumu na Migori kulalamikia uamuzi huo. Waandamanaji hao pia waliteketeza gari huku wakiwasha moto kwenye barabara zinazoelekea kwenye eneo la katikati mwa jiji la Kisumu. Kituo kikuu cha mabasi mjini Kisumu kimekuwa mahame. Jaji mkuu David Maraga leo asubuhi amewasilisha uamuzi ulioafikiwa kwa kauli moja na majaji wa mahakama ya juu ambao ulitupilia mbali rufaa zilizowasilishwa na walalamishi wawili kutokana na kile alichokitaja kuwa kukosa uzito na hivyo kudumisha kuchaguliwa tena kwa Uhuru. Jiji la Kisumu limeshuhudia ghasia katika miezi michache iliyopita tangu uchaguzi mkuu wa tarehe nane Agosti huku wati kadhaa wakiripotiwa kufariki. Kaunti hiyo ilisusia marudio ya uchaguzi wa urais tarehe 26 mwezi uliopita.