Chama cha madaktari chapongeza uteuzi wa Nanok

Chama cha madaktari na wataalam wa meno nchini-KMPDU kimeeleza kuridhishwa na uteuzi wa gavana wa Turkana Josphat Nanok kuwa mwenyekiti mpya wa baraza la magavana. Kupitia mtandao wake wa Twitter, chama hicho kinasema Nanok atakita uadilifu katika kuimarisha uhusiano na wahudumu wa afya katika serikali za kaunti. Aidha ujumbe huo unasema gavana Nanok amedhihirisha katika kaunti yake ya Turkana jinsi uhusiano mzuri wa kikazi unaweza kuimarisha utoaji huduma za afya katika kaunti.Nanok alichaguliwa jana kuchukua mahala pa gavana wa Meru, Peter Munya, baada ya muhula wake kukamilika. Wakati huo huo, uteuzi wa Nanok kuwa mwenyekiti wa baraza la magavana pia umepokewa kwa furaha na wafuasi wake katika kaunti ya Turkana. Wanaolelea uteuzi wake kuwa ishara ya kuwa na imani na tajriba yake ya uongozi. Huku furaha ikitanda mjini Lodwar, wakazi walitaja uteuzi wa gavana huyo wa chama cha ODM kwa wadhifa huo wa kifahari kuwa baraka nyingine kwa jamii ya Waturkana na taifa lote kwa jumla. Gavana wa taifa Taveta John Mruttu alidumisha wadhifa wake wa naibu wa mwenyekiti ilhali gavana wa Kiambu, William Kabogo, sasa ndiye kiranja mkuu mpya. Uchaguzi huo uliandaliwa jijini Nairobi jana.