Utata Waibuka Kuhusu Makubaliano Ya Wanajeshi Wa Uingereza Kuendelea Na Mafunzo Nchini Kenya

Wasiwasi unaibuliwa kuhusiana na kuendelea kuafikiwa upya kwa makubaliano ya kuruhusu kitengo cha wanajeshi wa Uingereza kufanya mazoezi nchini Kenya.A� Mpango huo umekuwa ukitekelezwa tangu wakati wa ukoloni chini ya makubaliano ambayo yanafikiwa upya kila baada ya miaka mitano. Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa amesema kwamba wanajeshi hao wamesababisha masaibu mengi kwa wakazi wa sehemu zilizoko karibu na vituo vyao vya mafunzo katika kaunti za Laikipia na Samburu. Kwa muda mrefu makubaliano hayo yameruhusu kitengo cha vita cha wanajeshi wa Uingereza kutoa mafunzo kwa wanajeshi wake katika mazingira ngumu nchini Kenya kujiandaa kwa Oparesheni hatari sana.A� Wanajeshi hao wamedaiwa kuwabaka wanawake na kuacha vilipuzi chini ya ardhi katika viwanja vya mafunzo ambavyo vimewaua na kulemaza watu wengi katika sehemu hizo. Jamii ya Wa-Samburu pia imelalamikia kuharibiwa kwa malisho yao ya mifugo kwa kugeuzwa kuwa viwanja vya mafunzo vya wanajeshi hao. Akiongea wakati wa mkutano wa kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi huko Nanyuki,Wamalwa aliye pia mwanachama wa kamati hiyo alisema kwamba wakenya sharti wahakikishe manufaa kwao kuhusiana na kuafikiwa upya kwa makubaliano hayo. Mbunge huyo alitaka kufahamishwa masharti ya ubadilishaji wa Tekinolojia na jinsi makukubaliano hayo yanawafaidi wakenya. Hata hivyo mwenyekiti wa Kamati hiyo Ndunga��u Githenji alisema kwamba kuafikiwa upya kwa makubaliano hayo kutazingatia maslahi ya jamii zinazoathiriwa. Mbunge wa Tetu alisema kwamba harakati za kuafikiwa kwa makubaliano hayo zitashirikisha umma kabla ya kuwasilishwa bungeni.