Usambazaji wa vitabu kwa shule za sekondari kukamilika Ijumaa

Usambazaji wa vitabu vya kiada kwa shule za upili za umma unatarajiwa kukamilika siku ya Ijumaa.A�Kuambatana na mpango huo wa serikali, wanafunzi wote wanaojiunga na kidato cha kwanza watapata vitabu vya masomo muhimu ya Hisabati, Kiingereza, Kiswahili, Kemia, Fizikia na Biologia. Vitabu vya mwongozo kwa waalimu kuhusiana na mtaala mpya wa masomo vitawasilishwa kwenye shule hizo ifikapo mwisho wa juma.

Serikali inalenga kutumia shilingi bilioni 7.5 kufadhili mpango wa utoaji vitabu vya ziada moja kwa moja shuleni. Vifaa na vitabu vya mafunzo ya mtaala mpya wa elimu vinatolewa na tasisi ya ustawishaji mtaala ikishirikiana na wachapishaji vitabu. Shughuli hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu uliozinduliwa na serikali mwaka 2017 wakati awamu ya majaribio ilipoanzishwa kwenye shule 10 katika kila kaunti humu nchini. Shule hizo zinajumuisha zile za umma, za binafsi na za wanafunzi walio na mahitaji maalum. Kundi la kwanza la wanafunzi wa kidato cha kwanza linatarajiwa kuripoti shuleni hapo kesho ilhali kundi la mwisho linatarajiwa kuripotiA� kufikiaA� tarehe 12 mwezi ujao .