Usalama Waimarishwa Katika Kaunti Za Lamu Na Tana River

Vituo kadha vipya vya polisi vimezinduliwa katika maeneo yenye usalama duni katika kaunti za Lamu na Tana River kukabiliana na vitisho vya kigaidi.Vituo vitatu vya polisi vimefunguliwa katika sehemu za Bothei, Pandanguo  na  Mananguo  kama sehemu ya hatua  za kuimarisha usalama.Milingoti mitatu ya mawasiliano ya simu pia imewekwa katika sehemu hiyo kuimarisha mawasiliano baina ya wakazi na maafisa wa usalama.Kwengineko,naibu mmoja wa kamishna wa kaunti na wasaididizi 12 wa makamishna hao wamepelekwa  huko  Ijara, Hulugho, Lamu mashariki na Lamu magharibi kama juhudi za kudumisha amani.Mkuu wa maafisa wa usalama walioko katika sehemu hiyo James Ole Serian alisema vituo kadha vya polisi pia vimekarabatiwa. Serian aliongeza kwamba oparesheni dhidi ya wanamgambo wa   Al-Shabaab  kwenye msitu wa Boni Forest itaendelea na akawahimiza wafugaji kutoingia kwenye msitu huo.Magaidi wamekuwa wakitumia msitu huo kutekeleza mashambulizi katika eneo la pwani.