Usalama Waimarishwa Kati Ya Mpaka Wa Narok Na Migori

Usalama umeimarishwa kwenye mpaka wa kaunti za Narok na Migori kufuatia kuzuka upya kwa mapigano kati ya jamii mbili za eneo hilo. Kameshina wa kaunti ya Narok Moffat Kangi amesema kwamba maafisa wa polisi wa kitengo cha GSU na wale wa kukabiliana na wizi wa mifugo wamepelekwa katika eneo hilo la mpakani ambalo huathiriwa na wizi wa mifugo na visa vingine vya utovu wa usalama.A� Akiongea na waandishi wa habari jana asubuhi Kangi alisema kwamba mwanamume mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi siku ya Ijumaa katika sehemu ya Mandugu huko Trans Mara magharibi kwenye mpaka wa kaunti za Narok na Migori. Alisema mauaji hayo yanayoshukiwa kutekelezwa na watu kutoka upande wa Kuria ndio yamezua taharuki ya sasa katika eneo hilo. Alionya kwamba wale wanaochochea taharuki na ghasia katika eneo hilo la mpakani watachukuliwa hatua kali. Kameshina huyo alisema kwamba eneo la kiusalama la umbali wa Kilomita tano kwenye mpaka wa Kaunti ndogo za Kuria mashariki na Trans Mara magharibi litaendeleas kulindwa na maafisa wa usalama ili kupunguza taharuki za mara kwa mara kati ya jamii za Maasai na Kuria hadi amani kamili itakaporejea.