Usajili wa tume ya kutetea haki za binadamu KHRC wafutiliwa mbali

Usajili wa tume ya kutetea haki za binadamu nchini inayoongozwa na Profesa Makau Mutua umefutiliwa mbali. Mkurugenzi mkuu wa bodi ya ushirikishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali Fazul Mohammed alisema kuwa bodi hiyo iliafikia uamuzi huo baada ya kugundua kwamba tume hiyo inaendesha akaunti nne za benki kinyume cha sheria ambapo imekiuka kifungu cha 12 sehemu ya nne ya sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali. Tume hiyo pia inashtumiwa kwa kukosa na kukataa kulipa ushuru wa shilingi milioni-100 kwa halmashauri ya ukusanyaji ushuru nchini. Tume hiyo pia imekosolewa kwa kuwaajiri wataalamu bila vyeti halisi na pia kuficha kile ambacho bodi hiyo imesema ni marupurupu haramu kwa makamishna wa bodi ya tume hiyo.