Usajili Wa Raia Wa Kigeni Waibua Hofu Burundi

Serikali ya Burundi leo ilizindua harakati ya kuwasajili raia wote wa kigeni, hatua ambayo imeibua hofu kuwa huenda kuna njama ya kuwachunguza raia hao. Msemaji wa wizara ya usalama wa umma, Alain-Guillaume Bunyoni alisema raia wote wa kigeni wametakiwa kuripoti katika vituo vya polisi vilivyoko mpakani katika muda wa miezi miwili ijayo. Alain-Guillaume alikariri kuwa hatua hiyo inalenga kuwapa raia wa kigeni vitambulisho vya kisasa kwa urahisi. Raia hao wa kigeni watatakiwa kufika binafsi katika vituo hivyo vya polisi na kuwasilisha hati zao za kusafiria. Wakizungumzia kuhusu hatua hiyo,raia wa Rwanda walisema hatua hiyo huenda ikasababisha kudhulumiwa kwa wenzao walioko nchini Burundi. Maelfu ya raia wa Rwanda wametorokea nchini Burundi tangu nchi hiyo ilipokumbwa na mzozo wa kisiasa. Uhusiano kati ya Burundi na Rwanda umezorota huku serikali ya Burundi ikishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi nchini Burundi. Zaidi ya watu-400 wameuawa na zaidi ya wengine elfu-240 wametoroka nchini humo tangu kuzuka kwa mzozo huo mwezi Aprili.