Upinzani Wapongeza Hatua Ya Kutamatishwa Kwa Kesi Dhidi Ya Ruto Na Sang

Vinara wa Muungano wa CORD Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na seneta wa Bungoma Moses Wetangula wameridhia uamuzi wa mahakama ya kimataifa ya jinai ICC wa kutamatisha kesi dhidi ya Naibu wa Rais William Ruto na Joshua Sang. Katika taarifa kwa vyumba vya habari vinara hao watatu waliwapongeza wawili hao kwa kupata ushindi na kuwa huru kutokana na kesi zilizowakabili. Vinara hao walisema wanatumai kwamba kutamatishwa kwa kesi hizo za ICC sasa kutairejesha nchi hii katika shughuli za ujenzi wa taifa kwa umakinifu na kupanua nafasi ya kidemokrasia.A� Hata hivyo viongozi hao wa upinzani waliilaumu mahakama hiyo ya Hague kwa kushindwa kushughulikia swala la waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi kikamilifu. Walisema ICC ilichukua hatua kinusunusu kwa waathiriwa ambao walikuwa na matumaini ya kutekelezewa haki kwa ukatili uliotekelezwa dhidi yao. Wakati huo huo viongozi hao wa upinzani waliihimiza serikali kuanzisha utaratibu ulio wazi wa kuwalipa fidia waathiriwa. Kwa upande wake kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi alipongeza uamuzi huo wa kutamatisha kesi za wawili hao akisema kesi hizo zimekuwa kikwazo kwa uwezo wa wakenya kuzingatria maswala wa ujenzi wa taifa. Mudavadi alisema kwa kutamatishwa kwa kesi hizo serikali inapaswa kuzingatia kuwahudumia wakenya ipasavyo.