Umoja wa Mataifa watoa wito wa kuachiliwa huru kwa wahamiaji nchini Libya

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuachiliwa huru mara moja kwa wahamiaji wanaozuiliwa nchini Libya ambao wengi wao wametendewa unyama. Libya ilitumbikia kwenye lindi la ghasia baada ya Muammar Gaddafi kubanduliwa mamlakani mwaka-2011 huku makundi kadhaa ya wanamgambo yakichipuza kujaza ombwe la uongozi. Na mambo yameenda mrama nchini humo baada ya kuzinduliwa kwa serikali mbili pinzani na kulazimu maelfu ya raia kutorokea nchi za Ulaya. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema kwenye ripoti yake iliyonakiliwa kati ya mwezi Aprili na Agosti kwamba wahamiaji nchini Libya wanateswa, kubakwa na kufanyishwa kazi za usaragambo.