Umati Mkubwa Wakusanyika Kumzika Aliyekuwa Rais Wa Iran

Maelfu ya raia nchini Iran wamekusanyika mjini Tehran kwa mazishi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Akbar Hashemi Rafsanjani. Kiongozi wa kidini nchini Iran,A´┐ŻAyatollah Ali Khamenei atatekeleza sala za wafu katika chuo kikuu cha Tehran. Rafsanjani ambaye alikuwa rais wa Iran kuanzia mwaka 1989 hadi 1997 alifariki kutokana na mshtuko wa moyo mnamo Jumapili akiwa na umri wa miaka 82. Siku tatu za maombolezi zimetangazwa nchini humo kuanzia jana. Mazishi hayo yanatarajiwa kuwa kigezo cha umaarufu kati ya wapenda mageuzi na wasiopenda mabadliko. Hata hivyo wakereketwa wa kiislamu nchini humo wanatarajiwa kuhudhuria mazishi hayo kwa wingi kwani Rafsanjani alikuwa mmoja wao. Rais huyo wa zamani atazikwa karibu na kaburi la kiongozi wa mapinduzi nchini humo, hayati Ayatollah Khomeini. Rafsanjani alikuwa mwandani wa rais wa sasa Hassan Rouhani na aliunga mkono mpango wa nuklia kati ya Iran na nchi zenye uwezo mkubwa duniani. Wizara ya mashaiuri ya nchi za kigeni ya Marekani imemtaja Rafsanjani kuwa kiongozi shupavu katika historia ya Iran