Ulinzi Stars Kuchuana Na Al-Hilal Benghazi Ya Libya.

Waliokua mabingwa wa ligi kuu ya soka ya Sportpesa, Ulinzi Stars wanatarajiwa kuelekea jijini Cairo, Misri Jumatatu ijayo, ambako watachuana na timu ya Al-Hilal Benghazi ya Libya, katika mechi ya raundi ya kwanza, mkondo wa kwanza, kuwania taji la mashirikisho ya soka Barani Afrika tarehe kumi mwezi ujao, katika uwanja wa chuo cha majeshi jijini Cairo. Mechi hiyo ambayo itachezwa bila mashabiki haingeandaliwa nchini Libya kutokana na sababu za kiusalama. Naibu wa mwenyekiti wa kilabu hicho Meja Joe Birgen, alisema ana matumaini kikosi hicho kitaandikisha matokeo chanya dhidi ya timu hiyo ya Afrika Kaskazini. Ulinzi Stars ilitoka sare na Mathare United bao moja kwa moja katika mechi ya kujipima nguvu iliyochezwa katika uwanja wa Gatuzi la Machakos, mwishoni mwa juma. Wakati uo huo, mabingwa wa ligi kuu ya Sportpesa, Tusker wanajiandaa kucheza mechi ya raundi ya kwanza,mkondo wa kwanza, wa ligi ya kilabu bingwa barani Afrika dhidi ya mabingwa wa soka nchini Mauritania, AS Port-Louis 2000 tarehe 11 mwezi ujao, jijini Porta��Louis.