Uhuru na Raila kuhudhuria maombi ya amani

Muungano wa madhehebu ya Ki-evanjelisti hapa nchini kesho utaandaa ibada maalum katika bustani ya Uhuru jijini Nairobi kuombea amani idumu hapa nchini kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi agosti. Kwa mujibu wa mwandalizi wa maombi hayo, askofu John Warari Wakabu, mgombea urais wa chama cha Jubilee, Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga watahudhuria ibada hiyo. Maombi hayo ambayo yataanza mwendo wa saa nne ni muhimu zaidi wakati huu ikizingatiwa utepetevu wa viongozi wa kidini wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka-2007 uliozongwa na ghasia. Askofu Warari aliliambia shirika la utangazaji la KBC kuwa kanisa linasikitika zaidi kwa kutotekeleza wajibu muhimu wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka-2007.