Uhuru Kenyatta na Raila Odinga wapongezwa na umoja wa mataifa

Umoja wa Mataifa umepongeza juhudi za rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa NASA, Raila Odinga za kuzindua mashauriano ya kuwaunganisha Wakenya. Kwenye taarifa, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kuunga mkono na kushirikiana na serikali na raia wa Kenya katika juhudi za kuimarisha amani, uthabiti na maendeleo. Guterres alielezea kuridhishwa kwake na taarifa ya pamoja ya rais Kenyatta na Raila Odinga Ijumaa iliyopita ambapo walijitolea kushirikiana na kuimarisha umoja wa Wakenya akisema hiyo ni hatua kubwa ya kutafuta suluhu la kudumu kwa matatizo ya kisiasa yanayoghubika nchi hii. Rais Kenyatta na Raila walifanya mkutano ambao haukutarajiwa katika jumba la Harambee ambapo waliafikiana kukomesha mashindano ya kisiasa yaliochochewa na uchaguzi mkuu wa mwaka uliopita. Miongoni mwa masuala ambayo viongozi hao wawili wanapanga kushughulikia ni kukomesha uhasama wa kikabila, kukuza maadili ya kitaifa na kutokomeza zimwi la ufisadi. Malengo yao ni kuwajumuisha wakenya wote kwenye mfumo wa utawala, kufanikisha ugatuzi, kuimarisha usalama, ugavi sawa wa rasilimali na kuzingatia haki za raia.