Uhuru Kenyatta atuma risala za pongezi kwa George Weah

Rais Uhuru Kenyatta ametuma risala za pongezi kwa George Weah aliyeshinda uchaguzi wa urais nchini Liberia. Rais Kenyatta pia aliwapongeza raia wa Liberia kwa kufanya uchaguzi wa amani na akaahidi kuendelea kushirikiana na rais mteule. Kwenye ujumbe wake kwenye kitandazi cha twitter, rais Kenyatta alisema Kenya itaendelea kuungana na Liberia kuhimiza umoja wa bara Afrika kwani ndio njia pekee ya kudumisha ustawi wa bara hili. Weah anachukua mahali pa Ellen Johnson Sirleaf, hii ikiwa ndiyo mara ya kwanza kwa taifa hilo kupokezana madaraka kidemokrasia. Naibu wa rais atakuwa Jewel Howard-Taylor, mke wa zamani wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Charles Taylor ambaye anatumikia kifungo cha miaka 50 gerezani nchini Uingereza baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu wa kivita.