Uhuru awarai wakazi wa Garissa kumpigia kura

Rais Uhuru Kenyatta amewarai wakazi wa kaunti ya Garissa kujitokeza kumpigia kura juma lijalo. Akiongea alipozuru kaunti hiyo, rais alisema serikali ya Jubilee imeanzisha miradi mingi ya Maendeleo katika eneo hilo ambayo itakamilisha ikiwa atashinda marudio ya uchaguzi wa urais. Rais aliwahimiza wakazi kupuuzilia mbali kile alichotaja kuwa sarakasi za mrengo wa NASA zinazolenga kuvuruga marudio ya uchaguzi wa urais na kuleta machafuko humu nchini. Rais pia alikosoa maandamano ya muungano wa NASA yanayoendelea katika baadhi ya miji humu nchini akisema ni njama ya wahuni ya kupora na kuharibu mali ya Wakenya wanaojitafutia riziki. Alitahadharisha kuwa wale watakaofumaniwa katika vitendo vya kihalifu watachukuliwa hatua za kisheria. Rais pia alizuru kaunti za Kitui na Machakos.