Uhuru awahakikishia wananchi maisha bora
Rais Uhuru Kenyatta amewahakikishia wananchi kuwa amejitolea kikamilifu kuwahudumia kuboresha maisha yao kwenye kipindi chake cha pili afisini. Akiongea aliposimama katika eneo la Githurai Kimbo, kaunti ya Kiambu, kupokea salamu za wananchi, Rais Kenyatta alisema kuwa atahakikisha kuwa miradi muhimu itakayoboresha maisha ya Wakenya haikawii kukamilishwa. Katika sehemu ya Githurai Kimbo na maeneo yamkaribu, Kenyatta alisema miradi itakayopewa kipa umbele ni ukarabati wa barabara, ujenzi wa masoko na usambazaji wa maji safi. Rais alisema atawasiliana na magavana Ferdinard Waititu wa Kiambu na mwenzake wa Nairobi, Mike Mbuvi Sonko ili kuhakikisha eneo la Githurai linapata soko jipya, huduma za maji na barabara. Aliongeza kuwa utawala wake utahakikisha eneo hilo linapata rasimali za kutosha ili kuboresha maisha ya wakazi wake. Rais alikuwa akirejea jijini baada ya kuhudhuria mazishi ya marehemu Charity Gathoni Muigai Kenyatta ambaye alizikwa katika shamba lake kwenye eneo la Githurai Kimbo. Marehemu Mama Charity Gathoni ni jamaa wa Rais.