Uhuru kuanzisha malipo ya kuwasaidia wafugaji

Rais  Uhuru Kenyatta wiki hii atazindua rasmi malipo ya pesa za kuwasaidia wafugaji kununua malisho ya mifugo wao hadi msimu wa  ukame uishe.  Wafugaji wasiojimudu katika kaunti za Mandera, Marsabit, Isiolo, Tana River, Turkana na Wajir watanufaika na malipo ya shilingi milioni  215. Malipo hayo chini ya mpango wa bima ya mifugo hapa nchini yanalenga kunufaisha familia 12,600 zilizosajiliwa za wafugaji katika kaunti saba. Msemaji wa ikulu  Manoah Esipisu amesema hayo leo katika ikulu ndogo ya  Sagana kaunti ya  Nyeri . Esipisu amesema serikali itaimarisha mikakati ya kukabiliana na athari za ukame katika kaunti 23. Alisema usafirishaji  wa maji umeimarishwa katika kaunti zilizoathirika na serikali imekarabati visima vya maji ambamo maji hayo yanatolewa.