Uhuru Ataka Wanasiasa Kuunga Mkono Mradi Wa Maji Mwea

Rais Uhuru Kenyatta amewataka viongozi wa kaunti ya Kirinyagah kukoma kuvuruga mipango ya serikali ya kuimarisha mradi wa Mwea wa kilimo cha unyunyiziaji mashamba maji. Rais alisema mpango huo wa serikali ya taifa wa kujenga bwawa kubwa ili kusambaza maji zaidi kwa mradi huo umetatizwa na wanasiasa. Akiongea jana alipozuru kaunti ya Kirinyagah, ambako mradi wa Mwea unapatikana, rais alisema serikali haitavumilia mwingilio wa wanasiasa kwenye mradi huo. Rais alisema serikali imetenga fedha za kutosha za kuimarisha mradi huo na wale walioachwa bila makazi kufuatia ujenzi wa bwawa hilo watafidiwa. Jumla ya shilingi bilioni 4.1 tayari zimelipwa kama fidia kwa wale walioachwa bila makazi kufuatia ujenzi wa bwawa hilo na ardhi ya ekari 350 pia imenunuliwa ili kuwapa upya makazi.