Uhuru apongeza Harambee Stars kwa kushinda dimba la mwaka, CECAFA

Rais Uhuru Kenyatta amepongeza timu ya taifa ya SOKA, Harambee Stars kwa kushinda dimba la mwaka huu la CECAFA senior challenge. Harambee stars ilitwaa kombe hilo baada ya kuishinda Zanzibar mabao 3 kwa mawili kupitia mikwaju ya penalti katika uwanja wa michezo wa Kenyatta huko Machakos. Rais Kenyatta aliwapongeza wachezaji pamoja na maafisa wa timu hiyo ya Harambee Stars kwa kazi nzuri iliyochangia ushindi huo. Kiongozi wa taifa alisema ushindi wa Harambee Stars umebaini kuwa kujitolea pamoja na matayarisho kabambe vitaweza kusaidia Kenya kuwa bingwa wa soka barani Afrika. Alikariri kujitolea kwake kukuza michezo kama njia kustawisha vipaji miongoni mwa vijana.