Ugonjwa Wa Saratani Huenda Ukasababisha Vifo Vingi Zaidi Hapa Nchini

skk

Ugonjwa wa saratani huenda ukawa ugonjwa unaosababisha vifo vingi zaidi hapa nchini iwapo serikali haitaharakisha upatikanaji wa vifaa vya kutibu ugonjwa huo. Gavana wa Pokot magharibi, Simon Kachapin ameelezea wasiwasi wake akitoa mfano wa kituo cha kutibu maradhi hayo cha Eldoret ambacho alisema hakihudumu.

Kachapin ambaye alikuwa akiongea wakati wa utoaji dawa za thamani ya shilingi milioni-48 kwa vituo mbali mbali vya matibabu katika kaunti hiyo, aliihimiza serikali ya kitaifa ihakikishe kwamba wagonjwa wa saratani hapa nchini hawaagi dunia kwa kutohamasishwa kuchunguzwa na kutibiwa ugonjwa huo mapema.

Gavana huyo alisema serikali yake inajitajidi kuhakikisha kwamba miundombinu ya afya imetolewa katika kaunti ya Pokot magharibi. Alifichua kwamba hospitali ya matibabu maalum ya kaunti hiyo imeajiri madaktari kadhaa wakiwemo wale wa matibabu maalum ili kupunguza gharama ya kuwapeleka wagonjwa katika hospitali ya matibabu maalum ya Moi.