Uchunguzi Kuanzishwa Dhidi Ya Ndege Ya Kampuni Ya EgyptAir Iliyotoweka

Uchunguzi umeanzishwa baada ya ndege moja ya shirika la ndege la Misri kutoweka jana katika bahari ya Mediterranean. Ndege hiyo nambari MS804 ilikuwa ikisafiri kutoka jijini Paris ufaransa ikielekea Cairo Misri, ikiwa imewabeba abiria 66 na wahudumu. Waziri wa ulinzi wa Ugiriki amesema kuwa mitambo ya rada ilionyesha kuwa ndege hiyo ilikuwa imepiga kona mara mbili na kurudi chini karibu fiti elfu 25, kabla ya kuanguka baharini. Misri imesema kuwa huenda ndege hiyo ilidunguliwa na magaidi. Oparesheni kubwa ya kuitafuta ndege hiyo inayojumuisha vikosi vya kijeshi vya Misri, Ugiriki, Ufaransa na Uingereza inaendelea karibu na kisiwa cha Ugiriki cha Karpathos. Maafisa wa kusimamia safari za ndege nchini Misri walikuwa wametangaza kuwa walikuwa wamepata sehemu ya mabaki ya ndege hiyo, lakini baadaye wakabatilisha taarifa hiyo. Ndege hiyo ilikuwa na abiria 56, wahudumu saba na maafisa watatu wa usalama.