Uchaguzi wa urais nchini Rwanda wafanyika leo

Raia wa Rwanda wanapiga kura leo kwenye uchaguzi wa urais ambapo rais Paul Kagame anatarajiwa kushinda kipindi cha tatu uongozini. Kagame mwenye umri wa miaka 59 anapingwa na Frank Habineza wa chama cha Democratic Green na mwaniaji huru Philippe Mpayimana. Kagame anasifiwa kwa kuleta maendeleo ya haraka ya kiuchumi tangu alipoanza kuhudumu mwaka 2000. Hata hivyo wakosoaji wanamshtumu kwa kukandamiza uhuru wa kisiasa. Shughuli ya uchaguzi kote nchini humo ilianza saa moja asubuhi na itakamilika saa kumi alasiri. Kagame anaakilisha chama tawala cha Rwandan Patriotic Front- RPF. Katiba ya nchi hiyo ilirekebishwa mwaka 2015, na hivyo kumpa Kagame fursa ya kuendelea kutawala hadi mwakaA� 2034. Wapinzani hao wawili wamelalamika kwamba wafuasi wao wanahofishwa hali ambayo wanasema inabainisha ni kwa nini ni watu wachache tu waliokuwa wakijitokeza kwenye mikutano yao ya kampeini.