Uchaguzi mpya kufanyika tarehe 17 Oktoba

Tume huru ya uchaguzi na mipaka-IEBC imetenga tarehe ya marudio ya uchaguzi wa urais kama ilivyoagizwa na mahakakama ya juu ijumaa iliyopita. Kulingana na tume hiyo ya uchaguzi, shughuli hiyo itaandaliwa tarehe 17 mwezi Oktoba mwaka 2017. Tume hiyo ya uchaguzi hata hivyo imesema kwamba ni majina ya rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa NASA, Raila Odinga yatakayokuwa kwenye karatasi za kura na hivyo haitawajumuisha wawaniaji wengine walioshiriki kwenye uchaguzi mkuu. Tume hiyo pia imesema kuwa inarekebisha masharti ya kuratibu na utekelezaji shughuli kabla ya marudio hayo ya uchaguzi wa urais na itashirikisha pande zote mbili na pia wadau kwenye taratibu hizo. Kadhalika tume hiyo inataka mahakama ya juu kuwasilisha maelezo kamili ya uamuzi wake ili kuiwezesha kujiandaa ipasavyo kwa uchaguzi huo. Tume hiyo imetoa wito wa nia njema kutoka kwa wadau ili kuiwezesha kuandaa uchaguzi ambao hautaibua shaka. Hata hivyo tume hiyo haijaashiria hatua zozote mashsusi itakazochukua kubadili makao yake makuu hata baada ya mwenyekiti wake Wafula Chebukati kuashiria hilo. Tume ya IEBC imekuwa ikikabiliwa na shinikizo kutoka kwa mirengo ya Jubilee na NASA kutangaza tarehe mpya ya uchaguzi huo kufuatia agizo la mahakama ya juu.