Ubomozi Wa Mijengo Haramu Wasimamishwa Nairobi

Serikali ya kaunti ya Nairobi imesimamisha kwa muda ubomozi wa mijengo yote haramu. Waziri wa ardhi wa serikali ya kaunti ya Nairobi Christopher Khaemba amesema maafisa wa serikali hiyo na wale wa serikali yaA� taifa watakutana kujadili njia mwafaka ya kutekeleza ubomozi huo huku kukiwa na hofu ya muingilio wa kisiasa kwenye shughuli hiyo. Khaemba alisema haya kufuatia ilani inayodaiwa kutolewa na afisa wa serikali ya kaunti hiyo Jumatatu hii ikiwataka wale wote ambao wamejenga nyumba za makazi katika mtaa wa Makongeni jijini Nairobi kuzibomoa ifikapo Ijumaa hii la sivyo watafurushwa. Hata hivyo Khaemba aliliambia shirika la KBC kuwa ubomozi wa mijengo isiyostahili utaanza katika muda wa mwezi mmoja ujao. Serikali ya kaunti ilitoa maagizo ya kubomolewa mijengo isiyostahili mnamo mwezi Mei mwaka huu kufuatia mkasa wa kuporomoka kwa nyumba ya makazi katika mtaa wa Huruma ambapo watu 51 waliuawa na wengine 400 kuachwa bila makao. Baadhi ya majumba yaliyoratibiwa kwa ubomozi huo yalikuwa yamejengwa bila idhini ya serikali ya kaunti ya Nairobi, Halmashauri ya kitaifa ya ujenzi na halmashauri ya usimamizi wa mazingira.