Uamuzi Wa Mahakma Dhidi Ya Kesi Ya Philip Tunoi

Kamati maalum yenye wanachama sita ya tume ya idara ya mahakama leo inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake ya uchunguzi kuhusu madai ya kupokea hongo dhidi ya jaji ya mahakama ya juu Philip Tunoi. Uchunguzi wa madai hayo ulianzishwa tarehe 27 mwezi uliopita baada ya jaji mkuu Dkt. Willy Mutunga kuthibitisha kwamba alikuwa amepokea taarifa ya kiapo kutoka kwa aliyekuwa mwanahabari ya kituo cha redio cha KASS, Geoffrey Kiplagat, akidai kuwa Tunoi alihongwa. Kiplagat aliwasilisha rufani akidai jaji huyo alipewa hongo la shilingi milioni 200 na gavana wa Nairobi Evans Kidero ili kumpendelea kwenye rufani iliyowasilishwa na Ferdinand Waititu baada ya uchaguzi mkuuA� mwaka wa 2013. Kamati hiyo inayoongozwa na Maragaret Kobia ilitarajiwa kuwasilisha matokeo ya uchunguzi wake kwa tume ya idara ya mahakama siku ya Jumatano lakini iliomba muda zaidi ili kuwasilisha uamuzi wake hii leo. Jaji Tunoi anakabiliwa na uwezekano wa kuchunguzwa na jopo ikiwa kamati hiyo itashawishiwa na taarifa ya kiapo ya Kiplagat na ushahidi uliowasilishwa. Lakini ikiwa kamati hiyo itashawishiwa na utetezi uliowasilishwa na jaji huyo, Kidero na wakili Katwa Kigen miongoni mwa wengine jaji Tunoi ataondolewa lawamani.