Turkey Yatangaza Siku Ya Kitaifa Ya Maombolezi

Uturuki leo imetangaza siku ya kitaifa ya maombolezi kutokana na shambulizi la bomu la kujitoa muhanga lililosababisha vifo vya watu 42,wakiwemo raia 13 wa kigeni kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Attaturk siku ya jumanne.Washambulizi hao watatu waliwasili kwenye uwanja huo kwenye teksi na kuanza kufyatua risasi kiholela kwenye lango la kuingia kwenye uwanja huo.Lakini walijilipua baada ya polisi kuwakabili.Waziri mkuu wa Uturuki Binali Yildirim alisema kuwa dalili za mwanzo zinaonesha kuwa wanamgambo wa Islamic state huenda walitekeleza shambulizi hilo.Hata hivyo kufikia sasa hakuna kundi lolote limedai kutekeleza uovu huo.Maafisa wa upelelezi wa Uturuki wanachunguza video za kamera za siri kwenye uwanja huo,na kuwahoji mashuhuda wa mkasa huo na abiria waliojawa hofu ,kubaini asili ya waliotekeleza shambuilizi hilo.Rais wa Uturuki Recep Tayip Erdogan alitangaza siku ya jumatano kuwa ya maombolezi ya kitaifa,huku akisema kuwa shambulizi hilo linachukuliwa kuwa kipindi muhimu katika vita dhidi ya makundi ya ugaidi duniani.Akizungumza katika mji mkuu wa nchi hiyo Ankara,Erdogan alisema kuwa licha ya taifa hilo kulengwa na mashambulizi katili zaidi ya kigaidi,limejitoa vilivyo kuangamiza ugaidi,huku akisema kuwa waliotekeleza shambulizi hilo si waislamu.