Tume ya polisi yalalamika kuhusu utekelezaji wa malipo ya mishahara mipya

Tume ya huduma ya taifa A�ya polisi imemwandikia barua inspekta jenerali wa polisi, Joseph Boinnet, ikisimamisha utekelezaji malipo ya mishahara mipya kwa maafisa wa polisi ambao wameongeza masomo yao. Barua hiyo iliyotiwa saini na afisa mkuu wa tume hiyo, Joseph Onyango, ilisema wamepokea malalamishi kutoka kwa maafisa wa polisi ambao wanaonelea kwamba hatua hiyo ya kuwaongeza mishahara wenzao ni ya ubaguzi. Tume hiyo imesema kwamba mabadiliko yoyote kwenye viwango vya mishahara lazima yatekelezwe kulingana na utaratibu uliowekwa baada ya visa kama hivyo kuchunguzwa na tume hiyo. Tume ya huduma ya taifa ya polisi miongoni mwa mambo mengine inashughulikia maslahi ya maafisa wa polisi. Tume hiyo ilisema imepokea malalamishi dhidi ya hatua hiyo ya kuweka viwango tofauti vya mishahara ya maafisa wa polisi ambao hali yao imebadilika baada ya kulemaa.