Tume Ya Kuthibiti Sekta Ya Kawi Nchini Yatangaza Ongezeko la Bei Ya Mafuta

Bei ya mafuta ya Super imeongezeka kwa shilingi 6 kwa lita kufwatia bei mpya zilizotangazwa na tume ya kuthibiti sekta ya kawi nchini ERC. Bei ya lita moja ya diesel imeongezeka kwa shilingi 9 huku ile ya mafuta taa ikiongezeka kwa shilingi 3 na centi 41 kwa kila lita. Bei hizo ziliaanza kutekelezwa saa sita za usiku jana hadi tarehe 14 mwezi ujao. Kuanzia jana saa sita za usiku, bei ya diesel itakuwa shilingi 83.24 kwa lita, petroli kwa shilingi 92.93 kwa lita na mafuta taa kwa shilingi 61.45 kwa lita jijini Nairobi.
Tume ya ERC imesema katika mabadiliko ya bei mwezi huu ilitilia maanani ada ya ziada ya shilingi 6 kwa lita ya ukarabati wa barabara kwa mafuta ya Super na diesel. Waziri wa fedha Henry Rotich alitangaza kuongezwa kwa ada ya ukarabati wa barabara kutoka shilingi 12 hadi 18 kwa kila lita ya petrol na diesel ingawa mabadiliko hayo hayakutekelezwa mara moja kwenye bei za mafuta. Ongezeko hilo la bei pia limechochewa na bei za juu za mafuta ambayo hayajasafishwa duniani.