Tume ya jinsia na usawa imesema kufungwa kwa madaktari kumezua mzozo katika sekta ya afya

Tume ya kitaifa kuhusu jinsia na usawa imesema kufungwa jela kwa maafisa wa chama cha madaktari kumezidisha mzozo katika sekta ya afya. Tume hiyo imeelezea wasi wasi wake kwamba watoto, wanawake, wazee na watu walio na ulemavu hawawezi kupata huduma za matibabu huku pande kwenye mzozo huo zikionekana kudumisha misimamo yao mikali.  Tume hiyo imesema hatua hiyo ni kinyume cha kifungu 43 (1) (a) cha katiba ya Kenya inayosema kila mtu ana haki ya kupata huduma bora za afya. Tume hiyo imesema jukumu kubwa katika kutatua mzozo huo limo mikononi mwa serikali zote. Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na mwenyekiti wa tume hiyo,  alisema juhudi zote zinapaswa kutekelezwa kutatua mzozo kati ya serikali na madaktari wanaogoma hata ikiwa italazimu maafisa hao kuachiliwa huru kutoka gerezani. Alitoa wito wa kurejelewa kwa mazungumzo ambayo alisema yanapaswa kufanyika kwa nia njema kwa lengo la kutatua mzozo huo kwa njia ya amani na inayofaa.